KILIMO CHA PAPAI
Papai ni tunda lenye ladha nzuri, na rahisi kuliwa. Aina hii ya tunda ni chanzo cha virutubisho muhimu mwilini, ambavyo husaidia kujenga mwili.
Zao hili asili yake ni ukanda wa kitropiki ambao hauna baridi kali na joto kiasi.
UDONGO
Mipapai hustawi vizuri kwenye udongo usiotuhamisha maji. Endapo maji yakituama kwenye eneo lililopandwa mipapai kwa muda wa siku mbili, mpapai unaweza kuoza kwa haraka na kufa. Kwa kuwa mipapai haina mzizi mkuu, inahitaji udongo wenye rutuba ya kutosha. Halikadhalika, zao hili halihitaji udongo wenye kina kirefu, hivyo ni muhimu kumwagilia mipapai wakati wa kiangazi. Wakati wa mapapai kuiva kama kuna ukame basi hali hiyo huongeza ubora wa papai ikiwamo kutooza mapema baada ya kuvunwa.
KUPANDA
Mipapai ipandwe sehemu ambazo hazina upepo mkali. Hii itasaidia mipapai kukua vizuri bila kuvunjika kwani mti wa mpapai huvunjika kirahisi. Inashauriwa kupanda miti ya kukinga upepo kuzunguka shamba la mipapai. Ili kuwa na tija zaidi, unaweza kupanda aina nyingine ya miti ya matunda kama vile miparachichi, na miembe.
Hakikisha miti ya kukinga upepo inakuwa mirefu kuzidi mipapai. Miti hiyo inaweza kutangulia kupandwa miezi kadhaa kabla ya kupanda mipapai.
MBEGU
Kusanya mbegu toka kwenye mapapai makubwa na yaliyo komaa na kuiva, kisha kausha mbegu vizuri kabla ya kupanda. Inashauriwa kununua mbegu kutoka kwa wazalishaji wanaoaminika na waliothibitishwa, ili kuwa na mazao bora zaidi na yanayoweza kukabiliana na magonjwa.
Mbegu aina ya red royal F1, inasifika zaidi kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na magonjwa yanayoshambulia mipapai, na huanza kuvunwa mapema zaidi, kati ya miezi 6 hadi 12. Aina hii huvunwa mfululizo kwa miaka 5 hadi 7.
UANDAAJI WA SHAMBA
Inashauriwa kuandaa shamba vizuri kwa kuondoa visiki na magugu yote. Shamba lilimwe vizuri, na kuhakikisha udongo umelainika vizuri.
MASHIMO
• Chimba shimo kwa ajili ya kupanda mpapai, liwe na kina cha sentimita 60 na upana wa sentimita 60.
• Weka mboji debe moja kisha changanya na nusu ya udongo uliotoa kwenye shimo, kisha rudishia kwenye shimo.
• Mwagilia maji kwa kipindi cha wiki mbili kabla ya kuotesha.
KUOTESHA
Sia miche kwenye kitalu, kasha hamishia shambani inapokuwa na urefu wa sentimita 30. Chomeka mche kwenye ardhi kina cha kati ya sentimeta 1 – 2 chini ya udongo kwenye shimo uliloandaa. Hii itasaidia mche kupata joto la wastani na kuepuka mche kuoza na kufa. Baadhi ya wakulima hupenda kuotesha mipapai moja kwa moja shambani.
Endapo unapenda kufanya hivyo, zingatia haya;
• Kabla ya kupanda mbegu weka mchanganyiko wa majivu na mbolea ya kuku au mboji sehemu unayokusudia kupanda. Mbolea husaidia ukuaji haraka na jivu husaidia kukinga mipapai na magonjwa.
• Panda mbegu 3 – 4 kila shimo, hii ni kwa sababu miche mingine inaweza kufa kutokana na magonjwa, kuliwa na wadudu au ikaota mipapai dume.
NAFASI
Shimo hadi shimo, liwe na nafasi ya mita 3, na mstari hadi mstari mita 3. Hii itasaidia miche ya mipapai kukua vizuri bila kusongamana.
PUNGUZA MICHE
Baada ya miezi 3 – 5 tangu kupanda, mipapai itaanza kutoa maua na hapo jinsia ya mipapai itajulikana. Inapofikia wakati huo inabidi kupunguza mipapai mingine hasa midume.
Mipapai yenye jinsi zote isizidi asilimia 10 – 20 ya miche yote iliyopo shambani, na midume ibaki mmoja katika kila majike 25.
UTUNZAJI
• Weka kilo 2 – 5 za samadi kwenye kila mpapai kwa mwaka ili kuongeza ukuaji na uzalishaji.
• Mabaki ya mimea yanaweza kuwekwa kama matandazo. Hii ni muhimu zaidi kipindi cha kiangazi ili kuzuia unyevu usipotee.
• Chunguza mipapai mara kwa mara ili kuangalia kama kuna magonjwa, ing’olewe na kuchomwa au kufukiwa chini endapo itabainika kuwa na maonjwa.
• Unaweza kunyunyiza dawa zisizo na madhara za kukinga au kukabiliana na magonjwa ya ukungu na virusi.
KUPOGOA
• Kata matawi yote yatakayojitokeza pembeni ya mpapai. Hili lifanyike mapema kabla ya tawi kuwa kubwa.
• Ondoa mipapai yote ambayo hayakuchavushwa vizuri na ubakize yenye afya tu.
PALIZI
• Mipapai inapopandwa tu inaweza kuwekewa matandazo kuizunguka ili kuzuia uoataji wa magugu.
• Magugu yang’olewe yakiwa machanga.
• Epuka kuchimbua sana wakati wa palizi kwa kuwa mizizi ya mipapai huwa juu juu.
MAGONJWA
Zao la papai halina magonjwa mengi sana yanayoshambulia endapo litatunzwa vizuri. Hata hivyo kuna baadhi ya magonjwa ambayo yamezoeleka kwenye zao hili kama vile Ugonjwa wa madoa kwenye majani (Papaya spot) na Ugonjwa wa virusi unaojulikana kama Mozaic virus. Mimea yenye magonjwa inaweza kung’olewa na kufukiwa ili kudhibiti ueneaji kwenye mimea mingine.