TUTUMIE MVUA TUPANDE MITI KWA UTUNZAJI WA MAZINGIRA ILI TUENDANE NA MABADIRIKO YA NCHI.

Maeneo mbalimbali nchini yanapata mvua zinazowezesha wakulima kupanda mazao, pia zinapunguza joto na kupoozesha hali ya hewa mathalani jijini Dar es Salaam na mikoa mingine yenye hali ya joto kama hiyo, wananchi wanapata ahueni.

Hata hivyo, kwa muda mrefu kumekuwa na tatizo la ukosefu wa mvua kwenye mikoa mingi hali iliyosababisha kuongezeka kwa ukame na kuathirika shughuli za uzalishaji wa chakula, mazao ya biashara pia kuongeza taathira kwa mazingira.

Kukosekana kwa mvua kumesababisha maeneo mengi kuwa na ukame , shida ya maji kwa matumizi ya nyumbani na ya mifugo pamoja na kilimo.Lakini mvua zinavyonyesha huongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya nyumbani na mashambani.

Kwa wenye matangi ya kuhifadhia maji wanapata maji ya kutumia kwa muda mrefu huku maeneo ya wafugaji wanaotegemea malambo yanajaa na kuongeza uwezekano wa kupata hudumu hiyo kwa muda mrefu na kupunguza adha ya wananchi na mifugo kwenda umbali mrefu kutafuta maji.

Bila kusahau kuwa kwa kipindi cha ukame upandaji miti ni mgumu kwa kuwa haistahimili ukame lakini, kunapokuwa na mvua ardhi hupoa na mizizi inapenya na kujiimarisha kwenye udongo.

Hakuna ubishi kuwa Tanzania ni moja ya nchi zilizoathirika sana na uharibifu wa mazingira kwa vile watu hukata miti bila kupanda mingine licha ya kuwa na msukumo wa kufanya hivyo.

Athari za mabadiliko ya tabia nchi pamoja na mambo mengine, lakini kwa kiasi kikubwa ni uharibifu wa mazingira unaotokana na kukata miti , kufanya shughuli za kibinadamu kama kilimo karibu na vyanzo vya maji na ongezeko la viwanda vinavyozalisha hewa ukaa, huku kasi ya kuipunguza ikizidi kupungua kila siku.

Hakuna kiumbe anayeweza kuishi kwa amani na salama bila kuwa na mazingira salama ambayo ni yale yaliyotunzwa kwa kuwa na miti ambayo mbali na kupendezesha eneo husika hunyonya hewa chafu na kutoa nyingine safi inayotumiwa na binadamu.

Kwa umuhimu huo ni lazima kila mwananchi aione haja ya kupanda miti hasa katika msimu huu wa mvua, kwa kuwa itawezesha miti hiyo kushika ardhini na kuendelea kustawi hata msimu ambao hauna mvua.

Rai yangu kwa Watanzania ni kutumia mvua hizi kwa manufaa kwa kushiriki kampeni binafsi ya kupanda miti, kila mmoja apande mti na kufuatilia ukuaji wake kila wakati.

Hakuna namna tunayoweza kulisaidia taifa letu kuondoakana na jangwa kadhalika katika utunzaji wa mazingira bila kupanda miti kwa wingi ambayo itaondoa athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Vikundi mbalimbali vishiriki upandaji miti na kufuatilia maendeleo yake, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi wengi kushiriki kampeni hiyo.

Kwa dunia ya sasa Tanzania ni moja ya nchi inayoweza kuuza ‘gesi ya kaboni’ nje ya nchi kwa kuwa imeingia mkataba wa aina hiyo na nchi zenye viwanda vingi duniani, kwa mwenye eneo kubwa la miti anaweza kulitumia kama kitega uchumi kujipatia fedha za kumuwezesha kutatua mambo ya msingi kwa familia yake.

Miti ina faida nyingi ikiwamo matunda ya misimu mbalimbali, kivuli, kuhifadhi vyanzo vya maji, kusafisha hewa, kupendezesha maeneo hivyo tutafanikiwa kuyafurahia hayo iwapo kila mmoja kwa nafasi yake atapanda miti na kufuatilia ukuaji wake.

Wapo wanaoungana kwenye vikundi na kupanda miti lakini hakuna ufuatiliaji kiasi kwamba inakuwa bora liende walisikika kuwa walipanda miti.

Ni vyema viongozi kuanzia serikali za mitaa kuonyesha mfano kuanzia kwenye ofisi zao na nyumbani pia kuhamaisha wananchi kutumia mvua hizi kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Nakumbuka aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alipofika mkoani humo na kuona athari za uharibifu wa mazingira kiasi cha Moshi kuongoza kwa joto kali, alianza kampeni ya kupiga marufuku ukataji miti ovyo bali kwa kibali maalum na kila mwananchi kushiriki kampeni ya upandaji miti.

Jitihada hizo matokeo yake yanaonekana kwa sasa kwa kuwa mkoa huo una miti mingi na hali ya baridi kama zamani imeanza kurejea.

Aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Moshi mwaka 2010, Issack Kireti (SAU), moja ya ahadi yake kubwa ni kuupendezesha mji wa Moshi kwa miti ya matunda na alianza kidogo na sasa miti imesheheni katika barabara na mitaa mbalimbali.

Ni wajibu wetu kutunza mazingira kwa kupanda miti kwa kuendelea na kauli mbiu ya kata mti panda miti, ili kuhakikisha tunayafurahia maisha kila wakati.

Previous
Next Post »